TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars leo inashuka kwenye dimba la Royal Bafokeng nje kidogo ya Jiji la Rustenburg, Afrika Kusini kuikabili Swaziland kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kusini mwa Afrika (COSAFA) inayoendelea nchini Afrika ya kusini.
Taifa Stars ambayo ni timu mwalikwa katika michuano hiyo pamoja na Ghana, itacheza mechi hiyo kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Kusini, sawa na saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania.
Awali, michezo ya Kundi B ambalo Tanzania imo, ilikuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Olympia Park, lakini waandaaji wa Cosafa wamesema kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wao, michezo hiyo imeshindikana kufanyika hapo.
Uwanja wa Royal Bafokeng ni miongoni mwa viwanja viliyotumika katika fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini, ukiwa na uwezo wa kubeba watazamaji 42,000 huku timu ya Platinum Stars iliyopo Ligi Kuu ikiutumia kama uwanja wake wa nyumbani.
Jana Taifa stars ilifanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Rolay Bafokeng kwa ajili ya kuuzoea uwanja kabla ya mchezo wenyewe dhidi ya Swaziland.
Akizungumzia hali ya hewa, Kocha wa stars Martin Nooij alisema vijana wake wanaendelea kuizoea hali ya hewa, japokuwa kuna baridi hakuna mchezaji aliyeshindwa kufanya mazoezi kutokana na hali ya hewa.
Michuano hiyo ilianza jana kwa mechi mbili kati ya Namibia dhidi ya Shelisheli na Zimbabwe kuikabili Mauritius, wakati leo pia kutakuwa na me chi mbili ikiwamo ya kwanza kati ya Lesotho dhidi ya Madagascar.
Taifa Stars baada ya mechi ya leo itaikabili Madagascar keshokutwa, kabla ya kumalizana na Lesotho Ijumaa wiki hii,
Kikosi hicho cha Nooij kitaitumia michuano hiyo kama maandalizi ya michuano ya awali ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 ikianza na Misri, Juni 12, mwaka huu, kabla ya kuikabili Uganda katika michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN).
Nooij amekwenda na kikosi cha wachezaji 20 kwa ajili ya michuano hiyo ambacho kinajumuisha wachezaji wazoefu na chipukizi, na bila ya shaka, anategemea watampatia ushindi katika michuano hiyo.
Kikosi hicho kinawajumuisha makipa Deogratius Munishi na Mwadini Ali, mabeki ni Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Abdi Banda, Salum Mbonde na Haji Mwinyi.
Viungo ni Amri Kiemba, Salum Abubakar, Frank Domayo, Said Juma, Salum Telela, Hassan Dilunga, Said Ndemla, na Mwinyi Kazimoto wakati washambuliaji ni John Bocco,Juma Luizio, Ibrahim Ajib, Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
No comments:
Post a Comment