WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema ugonjwa wa zika haupo nchini, ingawa imesisitiza umma wa Watanzania kuchukua hadhari.
Waziri wa wizara hiyo Ummy Mwalimu alitoa taarifa hiyo jana kupitia kwa waandishi wa habari akiwataka wananchi kuondoa hofu kutokana na mashaka na hofu aliyosema yamejitokeza kwenye jamii juu ya kuingia kwa ugonjwa huo nchini.
Ingawa Serikali imeshatoa maelekezo kwa waganga wakuu wote wa wilaya, Waziri alisema wanasubiri mwongozo kwa kuwa kamati ya dharura ya miongozo ya kimataifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inalokaa leo mjini Geneva, Uswisi kufanya tathmini ya ugonjwa na kutoa maelekezo kwa nchi wanachama.
Alisema, baada ya kuwepo taarifa za ugonjwa, Serikali ilifanya ufuatiliaji katika vituo vyote vya kutolea huduma na mipakani kupitia mfumo uliopo na kubaini haujaingia nchini. “Tumejiridhisha kwamba ugonjwa wa zika haujaingia nchini.
Tumethibitisha na hadi jana (juzi) saa 9:00 usiku, taarifa za wizara za ufuatiliaji wa magonjwa zilieleza kuwa hakuna mgonjwa yeyote wa homa ya zika, hivyo wananchi wasiwe na hofu bali waendelee kuchukua tahadhari,” alisema.
Ugonjwa huo unaoenezwa na mbu aina ya Aedes unasababishwa na kirusi cha zika. Dalili zake zinatajwa kufanana na za homa ya dengue ambazo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na kupata vipele vidogo vidogo kama harara.
Dalili hizo huanza kujitokeza kuanzia kati ya siku mbili hadi saba tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha Zika.
Waziri alisema unatibika iwapo mgonjwa anapelekwa mapema hospitali na kupatiwa matibabu ya haraka ingawa alisema, hakuna dawa maalumu wala chanjo, isipokuwa mgonjwa hutibiwa dalili zinazoambatana.
No comments:
Post a Comment