Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limeamua kumteua mtaalamu wa kuchunguza maovu wanayotendewa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakizidi kushambuliwa kwenye nchi za Afrika Mashariki.
Baraza hilo la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 47 lilipitisha azimio kwa kauli moja la kuundwa wadhifa wa mtaalamu wa kuchunguza maovu dhidi ya Albino ambaye atahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Baraza hilo limeeelezea wasiwasi mkubwa kutokana na mashambulizi na mauaji ya kikatili dhidi ya Albino wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na wazee.
Azimio hilo liliwasilishwa na Algeria kwa niaba ya kundi la mataifa ya bara la Afrika baada ya Mkuu wa Kamisheni ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein mapema mwezi huu kulaani vikali mashambulizi dhidi ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi ambayo alisema yameongezeka katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kiasi cha watu 15 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa nchini Tanzania, Malawi na Burundi na albino wengine wametekwa nyara, kujeruhiwa kwa kakatwa viungo vya mwili na wengine wamelazimika kuyatoroka makaazi yao kuepuka ukatili huo.
Mashambulizi dhidi ya Albino huwa mara nyingi yanachochewa na imani za kishirikina kutokana na dhana potofu kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi husaidia mtu kupata utajiri.

.jpg)

.jpg)
No comments:
Post a Comment