HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA ALIPOKUWA ANAWASILISHA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

Leo ni usomaji wa bajeti ya nchi kwa mwaka 2015/16 ambayo ni bajeti ya mwisho kwa kipindi cha awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, pia bajeti hii itasomwa sambamba
nchi zote zilizomo kwenye jumuiya ya Afrika mashariki kasoro nchi ya Burundi ambayo mwaka wake wa fedha ni tofauti.

=========
Misamaha ya kodi: Serikali imekuwa ikipunguza misamaha ya ridhaa kupitia kwa waziri, sasa itapunguza kodi kwenye bidhaa muhimu kama tiba na bidhaa za mitaji na haitahitaji ridhaa ya waziri. Lengo kuu ni kupunguza mianya ya upendeleo hata rushwa kwenye misamaha ya ridhaa. Wizara ya fedha inaendelea kutangaza misamaha yote inayotolewa ili kuweka uwazi na taarifa zinapatikana katika tovuti ya wizara ya fedha.

Dhamira ya kuongeza mapato ya kodi: Kwa sasa makusanyo ya kodi ni takribani 12% ya mapato yote, utendaji wa TRA utapimwa, tutajitahidi kuziba mianya ya kukwepa kodi, matumizi ya mifumo itapunguza mianya ya kukwepa kodi na itabidi kasi ya kusambaza mifumo hii iongezwe.
Serikali haitafanya biashara na wafanyabiashara wasiotumia EFD, lazima sasa mfumo wa kielectroniki utumike kwa ajili ya malipo yote ya serikali ikiwemo faini mahakamani, viingilio mbuga za wanyama na nk na lazima maafisa maduhuli wasimamie hili. Tunaongeza kasi ya kufanya tathmini ya majengo mijini ili kupata tozo sahihi.

Itapitia upya viwango vya posho za safari katika mashirika ya umma, mikataba ya ukusanyaji kodi pia itapitiwa upya.
Kuimarisha usimamizi wa matumizi, serikali itaendelea kusimamia zabuni na utoaji wa fedha za mafungu kulingana na mapato.

Madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii: Serikali inayatambua na katika mwaka huu wa fedha serikali imedhamiria kulipa madeni, serikali itauza hati fungani kutambua madeni na kuimarisha hali ya fedha ya mifuko.

Sera za bajeti kwa mwaka 2014/15 zilijikita katika kukuza uchumi, kudhibiti mfumuko ya bei, kupunguza misamaha ya kodi na kujikita kuongeza mapato. Jumla ya trilioni 8.6 zilikusanywa sawa na asilimia 86 ya makadirio, tunakadiria kufikia asilimia 91 ya malengo ya jumla mpaka mwaka huu wa fedha kwisha. Mapato yasiyo ya kodi yatafikia asilimia 74.

Kwa ujumla anazungumzia bajeti inayoisha ikiwemo malengo waliyoyaweka, walipofikia hadi sasa na wanapotarajia kufika mpaka ukomo wa bajeti husika utapofika rasmi. Anasema sera za matumizi zimefikiwa ikiwemo mgao wa matumizi kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti.

Ubia kati ya serikali na sekta binafsi Miradi kadhaa ilitambuliwa ikiwemo Mabasi kasi, upanuzi bandari ya Dar es Salaam
Deni la taifa: Msisitizo umewekwa kukopa mikopo yenye masharti nafuu na deni la taifa limefikia 19.5. Ongezeko limesababishwa na uhitaji na kushuka kwa shilingi dhidi ya dola ya kimarekani. Kati ya hizo Deni la nje ni 73% na la ndani ni 26.8%.

Changamoto tulizokabiliana nazo ni mahitaji makubwa ya fedha kuboresha miundombinu, utegemezi wa mashirika ya umma ikiwemo TANESCO, TRL na mengineyo ambayo yalitakiwa yazalishe, mabadiliko ya tabia nchi, kuimarika kwa dola ya Marekani na kadhalika.

Utekelezaji wa bajeti kwa miaka mitano: Tumejenga vinu vya gesi, usambazaji umeme vijijini umeongezeka, tumeboresha miundombinu na uchukuzi, maboresho ya uchukuzi wa anga ikiwemo kuboresha viwanja na reli. Kuboresha sekta ya kilimo, kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu kwa kuongeza mikopo elimu ya juu, kuongeza walimu shule za msingi.
Usimamizi wa uchumi, kiwango cha ongezeko kimepanda na tumefanikiwa kupunguza mfumuko wa bei pia tumeweza kuongeza ajira ikienda sambamba na ongezeko kwa pato la taifa. Uwekezaji kutoka nje umeongezeka.

Thamani ya shilingi ilipungua kwa kasi zaidi mwishoni mwa mwaka 2014, ilisababishwa na kuimarika dola ya marekani, kushuka kwa bei ya dhahabu katika siko la dola, kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya dola, mauzo madogo nje, serikali inajizatiti kuimarisha thamani ya shilingi. Watu waupuke kuagiza bidhaa ambazo zinaweza kupatikana ndani pia tunaimarisha uuzaji wa bidhaa nje.

BAJETI YA MWAKA 2015/16
Huu ni mwaka wa kukamilisha mipango tuliyojiwekea na kujiwekea malengo ya miaka mitano ijayo tutajikita katika uchaguzi mkuu, umeme vijijini, maji vijijini na kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea pamoja na kuwekeza kwa rasilimali watu.
Sekta ya gesi inategemea kiliingizia taifa pato miaka ijayo na ajira kwa wananchi, hata hivyo sekta hio inakabiliwa na changamoto nyingi na serikali imeandaa sera kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na gesi kwa kuanzisha mfuko wa gesi na maandalizi ya kutunga sheria kuhakikisha usimamizi yataletwa bungeni. Sasa anaomba marekebisho wa baadhi ya sheria za kodi.
===
HITIMISHO
110. Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha hotuba yangu napenda kusisitiza mambo sita: Kwanza, Serikali imejizatiti katika ukusanyaji wa mapato ili Bajeti hii itekelezwe kama ilivyopangwa. Hatutamvumilia yeyote atakayekwamisha azma hii ya Serikali. Sisi viongozi tuwe mstari wa mbele katika kulipa kodi na kuhakikisha hatutumii mamlaka na madaraka yetu kusaidia ukwepaji kodi.
Pili, ili kuhakikisha Waheshimiwa wabunge kupitia Muhimili wa Bunge wanasimamia utendaji wa mashirika ya umma ipasavyo pamoja na kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Waheshimiwa wabunge wote ambao ni Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma ujumbe wao utafikia ukomo ifikapo tarehe 30 Juni, 2015.
Tatu, Serikali inatambua kero na ugumu unaosababishwa na ulimbikizaji wa madai ya makandarasi, wazabuni na watumishi wa Serikali. Kuanzia mwaka ujao wa fedha Serikali italipa ankara za umeme na maji za Serikali kwa pamoja (Centrally) na fedha hizo zitatoka katika Mafungu husika. Kama nilivyoeleza, Serikali imeanza kukabiliana na tatizo hili na imedhamiria kulishughulikia kwa dhati.
Nne, suala la madeni ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii linashughulikiwa na litamalizika. Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inasimamia mifuko hii kuhakikisha inabaki kuwa himilivu na zaidi ya hapo Serikali iko makini kuhakikisha mafao ya wastaafu wote yanalipwa kwa wakati na kwa ukamilifu.
Tano, kama nilivyoeleza Serikali imeongeza kima cha chini cha malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 85,000 ambalo ni ongezeko la asilimia 70. Hii ni katika jitihada za Serikali kuboresha maisha ya wastaafu.
Na Sita, kwa kutambua mchango wa wazee katika Taifa letu, Serikali inakamilisha taratibu za kuwalipa mafao.
111. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwatakia kila la kheri Waheshimiwa Wabunge wote wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi wakiwemo waliotangaza nia katika Uchaguzi Mkuu. Kwa Watanzania wenzangu wote napenda nichukue fursa hii kuwahamasisha sote tujitokeze kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na tushiriki kupiga kura mwezi Oktoba 2015 kwa amani na utulivu.
112. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: