NI ngumu kubishana na takwimu za watu walioenda shule, hata kama haikuingii akilini. Kwa mujibu wa Kampuni ya Utafiti ya CIES Football Observatory, staa wa Chelsea, Eden Hazard, ana thamani kubwa katika soko la uhamisho kwa sasa kuliko staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Ripoti hiyo imepima thamani za wachezaji 100 bora duniani kwa sasa, huku ikidaiwa kuwa Hazard ambaye alitajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka England kutokana na kiwango chake bora msimu uliomalizika anaweza kuuzwa kati ya Euro 135 milioni hadi 148 milioni.
Dau hilo linamfanya staa huyo wa Ubelgiji awe nyuma ya staa wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi ambaye bei yake kwa jumla itakwenda kwa Euro 280 milioni sokoni wakati Ronaldo ambaye msimu uliopita hajashinda lolote dau lake ni Euro 113 milioni hadi 124 milioni.
Winga wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Raheem Sterling, ambaye anataka kuondoka Anfield katika dirisha hili, yupo katika orodha ya wachezaji 10 bora wenye thamani zaidi sokoni huku kiungo mahiri wa Chelsea, Cesc Fabregas, akikosa nafasi.
Fabregas ambaye pasi zake ziliisaidia Chelsea kutwaa ubingwa, ameshika nafasi ya 13 huku mshambuliaji kinda wa Tottenham aliyechipukia kwa kupiga mabao mengi msimu uliopita, Harry Kane, akishika nafasi ya 15.
Kane ambaye inadaiwa anasakwa na Manchester United kwa ajili ya kukipiga Old Trafford msimu ujao, amempiku winga wa Real Madrid, Gareth Bale, ambaye misimu miwili iliyopita alikuwa mchezaji ghali duniani.
Licha ya kununuliwa kwa dau la Pauni 85 milioni kutoka Tottenham misimu miwili iliyopita, thamani ya Bale imeshuka na sasa dau lake limewekwa kuwa Euro 58 milioni kwa mujibu wa CIES.
Kiungo staa wa Juventus na timu ya taifa ya Ufaransa, Paul Pogba, ambaye amekuwa akiwaniwa na klabu nyingi kubwa Ulaya, thamani yake imekwenda juu kufikia Euro 68 milioni na hivyo kuzionya Chelsea na Manchester City ambazo zimetajwa kumfukuzia kila wakati.
Pogba aliyeondoka Manchester United Julai 2012 kwa uhamisho wa bure kwenda Juventus, yupo katika orodha ya 10 bora akiwa ni mchezaji pekee kutoka Italia kuwamo katika orodha hiyo.
Mastaa wawili wa Barcelona ambao walifunga mabao mawili katika pambano la fainali la Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus Jumamosi iliyopita, Neymar na Luis Suarez, wapo katika orodha ya 10 bora huku Neymar akishika nafasi ya nne nyuma ya Ronaldo.
Kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois, ndiye mlindamlango ghali zaidi katika orodha hii akiwa anashika nafasi ya 18 kwa jumla baada ya kuwa na msimu mzuri katika lango la Chelsea na kumtoa katika nafasi ya kwanza kipa mkongwe, Petr Cech, anayetaka kuondoka.
Na katika hatua nyingine kiungo mahali wa zamani wa klabu ya fc Barcelona na timu ya taifa ya Hispania Xavi Hernandez ametambulishwa rasmi kwenye klabu ya mpya ya Al asaad ya nchini Qataar na kupewa jezi namba sita kama aliyokuwa anaitumia akiwa na miamba ya katalunya.
Xavi ameondoka Barcelona baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka 17 na kutwaa mataji zaidi ya 20 akiwa na klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment