STARS KIBARUANI LEO KUIKABILI UGANDA

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars leo inashuka dimbani kuikabili timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika za Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika Rwanda mwakani.

Huu ni mtihani wa kwanza kwa Kocha Mkuu, Mart Nooij ambaye baada ya kelele nyingi za mashabiki, shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) lilimpa mtihani wa mwisho kuwa ni kuivusha Tanzania kucheza fainali hizo na akishindwa, Mholanzi huyo atafukuzwa.

Tangu aanze kazi Aprili mwaka jana, Nooij ameiyongoza stars kwenye mechi 17, akishinda mechi tatu tu, kupoteza nane na kutoka sare saba, matokeo ambayo wapenzi wa soka nchini wanaamini hana jibu katika timu hiyo.

Stars itaikabili Uganda kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja leo saa mbili usiku. Taifa Stars imewahi kufuzu kwa fainali hizo mwaka 2009 ikiwa chini ya kocha kutoka Brazil, Marcio Maximo, fainali ambazo zilifanyika nchini Ivory Coast kuanzia Februari 22 hadi Machi 8 baada ya kuishinda Sudan kwa jumla ya mabao 5-2. Stars inahitaji ushindi katika mchezo huo wa awali ili kujiweka katika mzingira mazuri ya kusonga mbele, kabla ya mchezo wa marudaino utakaofanyika baada ya wiki mbili jijini Kampala.

Nooij alisema vijana wake wako katika hali nzuri na kuwaomba Watanzania kuwapa sapoti katika mchezo huo.
Endapo Stars itaitoa Uganda katika hatua ya awali, itafuzu katika hatua ya pili ambapo itacheza dhidi ya timu ya Taifa ya Sudan, na mshindi wa mchezo huo moja kwa moja atafuzu kwa fainali za CHAN 2016 nchini Rwanda.

Timu ya Taifa ya Uganda ilitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana mchana na kisha kwenda Zanzibar. Hata hivyo, mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu kwa Taifa Stars hasa kutokana na ukweli kuwa Tanzania imekuwa ikipata matokeo yasiyoridhisha dhidi ya Uganda.

Si hivyo tu, pia katika siku za karibuni Taifa Stars imepata matokeo mabaya katika mechi zake mbalimbali ikiwamo michuano ya Kombe la Cosafa na ile ya kufuzu kwa fainali za Afrika (Afcon) mwaka 2017.
Timu hiyo ilipoteza mechi zake zote tatu za makundi za Kombe la Cosafa nchini Afrika Kusini mwezi uliopita, kabla ya wiki iliyopita kufungwa mabao 3-0 na Misri katika kuwania kufuzu kwa Afcon 2017.

Kocha Nooij amewaongeza wachezaji watano ambao hawakuwa katika kikosi kilichocheza dhidi ya Misri kutokana na wachezaji wa kimataifa wa Tanzania kutoruhusiwa kucheza mchezo huo.

Waliongezwa ni Atupele Green, Hassan Isihaka, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa na Kelvin Friday, wanaungana na Deogratias Munishi, Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris na Nadir Haroub.

Wengine ni Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Mwinyi Haji, Abdi Banda, Frank Domayo, Amri Kiemba, Said Ndemla, Simon Msuva, na John Bocco.
Aidha, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetoa mwongozo kuwa mchezaji Mrisho Ngasa haruhusiwi kucheza CHAN kwa sababu sio mchezaji tena wa ndani.

No comments: