ZAWADI ZA LIGI KUU BARA MSIMU WA 2014/2015 KUTOLEWA LEO

ZAWADI kwa ajili ya timu zilizoshika nafasi za juu kwenye Ligi Kuu msimu wa mwaka 2014/2015 zinatarajiwa kutolewa leo na wadhamini wakuu wa ligi hiyo kampuni ya simu za mikononi ya vodacom.

Katika msimu huo, Yanga ndio ilitwaa ubingwa ikifuatiwa na Azam katika nafasi ya pili na Simba ikimaliza ya tatu na Mbeya City ikishika nafasi ya nne. Yanga kwa kutwaa taji hilo itazawadiwa kitita cha Sh milioni 80.4, Azam itapata Sh milioni 40.2, Simba Sh milioni 28.7 na Mbeya City Sh milioni 22.9.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa waandishi wa habari jana ilisema hafla hiyo iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, inatarajiwa kufanyika leo katika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio eneo la Posta Mpya jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni.

Taarifa hiyo ilisema mgeni rasmi katika hafla hiyo ya utoaji zawadi kwa wachezaji, makocha, na timu washindi ni Juma Nkamia, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Mbali na timu hizo zilizoshika nafasi nne za juu, Vodacom pia itatoa zawadi kwa mchezaji bora wa ligi, tuzo inayowania na Mohamed Hussein (Simba SC), Mrisho Ngasa na Saimon Msuva (Yanga

Kutakuwa na tuzo ya kipa bora inayowaniwa na makipa Mohamed Yusup (Prisons), Said Mohamed (Mtibwa Sugar), Shaban Kado (Coastal union).
Tuzo ya kocha bora inawaniwa na Goran Kopunovic (Simba SC), Hans Van Der Pluijm (Yanga) na Mbwana Makata - (Prisons).

Kwa upande wa mwamuzi bora, tuzo hiyo inawaniwa na Israel Nkongo, Jonesia Rukyaa na Samwel Mpenzu.
Tuzo ya timu yenye nidhamu inawaniwa na Mgambo , Mtibwa Sugar na Simba.

Kwa mujibu wa mkataba wa Vodacom, mfungaji bora atazawadiwa Sh milioni 5.7, sawa na kipa bora na mchezaji bora.
Timu yenye nidhamu itawazwadiwa Sh milioni 17.2, mwamuzi bora atapata Sh milioni 8.6 sawa na kocha bora.

No comments: