RAISI KIKWETE AWATEMBELEA NA KUWAPA POLE WAHANGA WA MVUA YA MAWE KAHAMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Machi 12, 2015, aliwatembelea na kuwapa pole wahanga wa mvua iliyoandamana na mawe na kusababisha upotevu wa maisha ya watu na uharibifu mkubwa wa mali katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.



















Rais Kikwete amewasili mjini Kahama kiasi cha saa nane mchana baada ya ndege yake kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mgodi wa Buzwagi na kwa muda wa kiasi cha saa tatu ametembelea familia ambazo zimepata madhara makubwa zaidi kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kwa kiasi cha saa moja tu kuanzia saa nne usiku Machi 3, mwaka huu, 2015 na kuambana na upepo mkali na mawe.


































Watu 47 walipoteza maisha, 112 waliumia, nyumba 657 zikabomolewa na kuharibiwa na kaya 468 kuathirika katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata na tokea siku ya maafa, Serikali imetoa huduma za dharura za chakula, sehemu za kulala, huduma za afya na huduma nyingine muhimu kwa binadamu.


































Rais Kikwete ataondoka leo, Ijumaa, Machi 13, 2015, kurejea Dar es Salaam baada ya ziara hiyo maalum ya siku mbili katika Mkoa wa Shinyanga.


No comments: