HAWA NDIO MAADUI 5 ATAKAOPAMBANA NAO MH PINDA AKIFANIKIWA KUWA RAISI WA TANZANIA

WAZIRI Mkuu Mh Mizengo Pinda jana alitangaza nia pamoja na kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya uraisi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu kupitia chama cha mapinduzi CCM

Pinda, ambaye amekuwa mgombea wa 32 kuomba fursa hiyo ndani ya CCM amesema Mungu pekee ndiye anayemjua mwanachama atakayeteuliwa kugombea nafasi hiyo, huku akitamani Mungu ampe kibali cha kuongoza Watanzania kwani ana lengo la kuwafikia wanyonge.

Pinda alifika Makao Makuu ya CCM saa nne asubuhi akiwa ameambatana na mkewe, Tunu Pinda, huku baadhi ya wabunge wakimsindikiza katika kumuunga mkono kwenye hatua yake ya kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuchukuwa fomu, Pinda alisema endapo atapata nafasi ya kushika nafasi hiyo ya juu nchini, atazingatia suala zima la mazingira na kuimarisha utawala bora, kwa kuwa hayo ndio nyongeza ya maadui watatu wa asili; ujinga, maradhi na umasikini.
“Ilani yetu haijatoka, humu ndipo kutakuwepo sera, maelezo na mikakati yote, kwa hiyo sina cha kusema mpaka Ilani itakapopitishwa na ikitokea nikateuliwa sitashindwa kuitekeleza na nalisema hili kwa uhakika.

“Kila aliyechukua fomu anataka ateuliwe yeye lakini Mungu pekee ndiye anayemjua, mimi simjui, na wala wenzangu hawamjui, na kila mmoja anasema moyoni mwake kwamba atakuwa yeye na Mungu angemnong’oneza basi angetamba mpaka asubuhi,” alisema.
Alisema katika kuimarisha utawala bora, atajikita katika kuimarisha Taasisi ya Kupambana na Kuzia Rushwa (Takukuru), ikiwa ni pamoja na kuwapa uhuru kamili katika kupambana na watendaji wasio waadilifu, wezi na wala rushwa.

“Watanzania wote tunawajibika kuhakikisha nchi inaongozwa kwa uwazi na kuwa na viongozi wenye maadili ambao wana uchungu na umasikini wa Watanzania.
“Tutaangalia jinsi ya kuipa meno Takukuru, wewe kama sio mla rushwa hauna haja ya kuogopa hili, mtu akipatwa apelekwe mahakamani hakuna hata haja ya kuomba kibali kwa Waziri Mkuu,” alisema Pinda.

Makada wengine waliokwisha kuchukua fomu ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo, mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe na Dk Hassy Kitine.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Dk Mwele Malecela, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kingwangala, Balozi, Amina Salum Ally, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.
Wengine ni Balozi Ally Karume, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Mtumishi wa CCM Idara ya Siasa na Uhusiano wa Tanzania Amos Siyantemi, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Wakili mwandamizi Mahakama Kuu Tanzania Godwin Mwapango, Peter Nyalile, Leonce Mulenda, Wengine Sospeter Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Makongoro Nyerere, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Robert, Balozi Agustino Mahiga na Monica Mbega.



No comments: