MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Yanga na wale wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Azam FC leo wanashuka dimbani kwenye viwanja viwili tofauti kujipima katika michezo ya kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.
Wakati Yanga wakicheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Azam FC watakuwa kwenye uwanja wa Aman Zanzibar saa moja jioni kuchuana na KMKM ya visiwani humo.
Kwa upande wa Yanga huo utakuwa ni mchezo wa pili wa kirafiki tangu wawasili Mbeya kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya ligi ambapo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Kimondo FC walifunga bao 4-1.
Yanga na Tanzania Prisons zilikutana mara ya mwisho kwenye michuano ya ligi ambapo Yanga waliibuka kidedea kwa mabao 3-1. Kikosi hicho cha Jangwani kinatarajiwa kuwatumia baadhi ya nyota wake ambao wamesajiliwa hivi karibuni akiwemo Mateo Simon kutoka KMKM, Mzimbabwe Thaban Kamusoko ambaye huo utakuwa mchezo wake wa pili.
Nyota wengine waliopo ni Donald Ngoma, Malimi Busungu, Geofrey Mwashiuya, Andrey Coutinho, Amis Tambwe, Haruna Niyonzima, Simon Msuva na wengine. Kabla ya mchezo huo Yanga walikuwa wachuane na Silva kesho lakini kutokana na taarifa ya Meneja wa timu hiyo Hafidh Salehe, timu hiyo ya Malawi imetoa udhuru.
Salehe alisema baada ya mchezo huo wa leo wanatarajiwa kucheza mchezo mwingine Jumapili dhidi ya Mbeya City. Kwa upande wa timu ya Azam FC mchezo wao dhidi ya KMKM ya Zanzibar utakuwa ni wa kwanza tangu wawasili Kisiwani huko.
Baadhi ya nyota ambao hawakuwepo akiwemo Didier Kavumbagu, Erasto Nyoni na Jean Mugiraneza tayari wameshawasili jana kujiunga na wenzao katika kambi hiyo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Azam Jaffar Idd, kikosi hicho kinaendelea vizuri kujifua na kwamba wanategemea kupata ushindi. Alisema mchezaji pekee ambaye hatakuwepo ni Allan Wanga ambaye alifiwa na mama yake mzazi.
No comments:
Post a Comment