MAANDIKO kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama mtemi Mkwawa
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad. Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo inatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Zuberi Suleiman Hamasi Mwawitala ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo
Shina la ukoo linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia Mwawitala anaanza kueleza. Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamududa. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamududa kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa. Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Mwawitala
Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.
Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.
Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe).
Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea.
Mwawitala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.
Inaelezwa kwamba, alipomfukuza, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.
Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao.
Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.
Utawala wa Munyigumba wapinduliwa na mkwewe
Utawala wa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tangu alipomuua kaka yake Ngawonalupembe mwaka 1860.
Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika Kijiji cha Lungemba akiwa amefanikiwa kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo zilizozaa kabila la Wahehe, wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni mtoto wake wa kwanza, alikuwa na umri wa miaka 24.
Kutokana na umri mdogo wa Mkwawa, ikabidi asikabidhiwe kwanza uchifu kwa wakati huo, hivyo ukoo ukamteua mdogo wake Munyigumba, Mtwa Mhalwike, aliyezaliwa na mke wa tatu wa Mtwa Kilonge, Mama Sekindole.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Mtwa Munyigumba kufariki na kutawazwa kwa Mhalwike, utawala huo ukapinduliwa na mmoja wa wafuasi wake na pia mkwewe aliyekuwa amemuoa binti yake. Mtu huyo, Mwamubambe Mwalunyungu, alikuwa anatokea eneo la Wassa na enzi za utawala wa Munyigumba ndiye hasa aliyekuwa kitumwa kazi ndogo ndogo kiasi cha kupendwa na hatimaye akapewa binti wa Chifu.
Huyu Mwamubambe kwa nini mdogo wake Munyigumba atawale? Nchi hii nitaichukua mimi mwenyewe.
Mwamubambe alimvamia Mhalwike kichakani, akampiga na kumchinja katika eneo hilo la Lungemba. Alipomaliza kazi yake hiyo haramu akaenda mahali ambako watu walikuwa wanakunywa pombe na kusema: Nchi hii ni yangu. Kama mnabisha nendeni kule kwenye miti mkamtazame Mhalwike Walipokwenda huko wakakuta maiti ya Mhalwike ikiwa imechinjwa kama kuku.
Wakati huo Mtwa Mkwawa alikuwa bado mdogo sana kupewa madaraka na kwa vile tayari Mwamubambe alikuwa ameupindua utawala, wakahisi Mtwa Mkwawa angeweza kuuawa kwa sababu ndiye mtoto mkubwa wa Munyigumba na ndiye hasa aliyetarajiwa kutawala. Hivyo, ikabidi wamkimbize kwenda kumficha Dodoma kwa Mtemi Mazengo wa Wagogo. Hii ndiyo sababu Wagogo wanawaita Wahehe wajomba zao na wanaheshimiana mno.
Wahehe hawakufurahishwa na utawala wa Mwamubambe anayechukuliwa kama adui mkubwa zaidi katika historia ya kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Kwa hiyo basi, wakapanga mbinu za siri kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.
Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa amejifunza mbinu za juu za kivita, akaamua kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwamubambe.
Hata hivyo, wapiganaji wengi wa Mtwa Mkwawa waliuawa na Mwamubambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa akitumia zaidi mitishamba kushinda vita nyingi kwa sababu hata dawa alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa na Mtwa Munyigumba, huku Mwamubambe mwenyewe ndiye akielekezwa kuzitafuta porini.
Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa na Mwamubambe, wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee Hee! Mtwa tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa ndipo lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa wakizipiga.
“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na kuwaua,
Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye ndoto akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena Mwakinyaga amwambie akamchome Mwamubambe kwenye kisigino au kidole.
Lundamatwe
Mwamubambe alikuwa na jeshi kubwa na wafuasi wengi wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili kuwapiga na kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwamubambe.
Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na wafuasi wa Mwamubambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama Lundamatwe (Lundika Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu ya Tanzam upande wa kusini.
Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga Ngondo Kimamula Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo aliamua kuchukua jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui zake.
Wapiganaji wa Mkwawa baada ya kuganguliwa wakaondoka kupambana na Mwamubambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga na kuwaua zaidi ya wapiganaji 1,000.
Mwamubambe alipoona mambo yamemzidia akatimua mbio, lakini wapiganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.
Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa na baba yake ndotoni kuhusiana na Mwamubambe, akaamua kumtuma Mukimayena Mwakinyaga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.
Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwamubambe anakunywa pombe. Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwamubambe akadondoka chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.
“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’ Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu, akamwambia; ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwamubambe akamwambia; ‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.
“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa kwamba akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini. Ndipo Mwamubambe akakata roho,
Mwamubambe alikuwa amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa kumbukumbu yake.
Baada ya hapo Mtwa Mkwawa akaendesha mapambano ya kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa Munyigumba, kampeni ambayo iliendelea moja baada ya nyingine kwa mafanikio makubwa kuliko hata awali.
HADI wakati huo, tayari von Heydebreck – mmoja wa manusura katika vita hivyo – alikuwa amekwishajeruhiwa na kuanguka akiwa amepoteza fahamu, lakini baadaye aliandika kwenye ripoti yake: “…Mfululizo wa matukio hadi wakati huu ulikuwa umetumia dakika mbili au tatu tu. Nilitambua hilo kabla ya kujeruhiwa, Wasudani tayari walikuwa wamekimbia kurudi nyuma vichakani baada ya kufyatua risasi mara mbili hivi. Mimi na askari wa Kikosi cha Tano tulilazimika kujilinda na kujitetea baada ya kuona Wahehe wakija katika umbali wa hatua 30. Kama sikosei, nilimsikia Sajini Tiedemann akisema alikuwa ameumia kabla hajafyatua risasi. Haikuwa rahisi kuona zaidi ya umbali wa hatua tano msituni kutoka pale njiani. Pia hakuna ambaye aliweza kunusurika kwa sababu Wahehe walikuja kwa kasi… Ni wazi walipanga kutushambulia baada ya kufika katikati msitu. Kuvurugika kwa mipango yao kulichangiwa hasa na kitendo cha Luteni von Zitewitz kufyatua risasi…”
Muanzilishi wa Himaya ya Ujerumani Afrika Mashariki, Carl Peters, baadaye Novemba 23, 1891 alimwandikia Gavana von Soden akisema kwamba, katika mapambano mengine na makabila mbalimbali ya Tanganyika, ilikuwa ni bahati tu kwao kutoweza kupata madhara kama waliyopata Wajerumani pale Lugalo, kwani mafunzo yao ya vita yalikuwa yanalenga zaidi kupigana wakiwa wamejipanga pamoja kwa mbinu maalum. Hawakuwa wamejifunza kupigana kila mtu kwa uwezo wake, bali walitegemea zaidi kushambulia kwa pamoja.
Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi) kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kupigwa nyundo kichwani akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia risasi wapiganaji wa Mkwawa. Kabla hajadondoka akachomwa mkuki ubavuni.
Hii ndiyo asili hasa ya jina la ‘Nyundo’ kutokana na kamanda huyo wa Wajerumani kuuawa kwa nyundo!
Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, kama Mjerumani Tom von Prince alivyoandika baadaye, “Kama nilivyosimuliwa baadaye… na Wahehe walioshuhudia, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kkihehe alipomchoma na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.”
Luteni von Pirch na Dk. Buschow pia waliuawa wakiwa juu wa punda wao ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha 6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.
Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.
Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. “Kulingana na ushuhuda wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na kuwaua maadui wengi (Wahehe).”
Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika 15 tu. Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili kuwaita manusura wengine.
Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha nyasi.
Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa zaidi ya 500.
Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.
Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.
Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO 62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo Agosti 29.
Hakuna takwimu halisi za idadi ya Wahehe waliokufa kwenye vita hiyo ingawa makadirio ni kati ya 260 hadi 700. Kwa ujumla, Wajerumani walikuwa wameshinda vita dhidi ya wakoloni, ushindi ambao ni wa kihistoria kwa mtawala yeyote wa Kiafrika wakati huo dhidi ya Wazungu. Haya yalikuwa matokeo mabaya zaidi kwenye vita katika historia ya ukoloni wa Wajerumani.
Jeshi la Wahehe halikuwa na haja ya kuhitimisha ushindi wake kwa kuwafuatilia Wajerumani waliosalia ili kuwaangamiza kabisa. Badala yake, kuanzia wakati huo wakaendelea kuishambulia misafara yote ya Wazungu.
BAADA ya ushindi wa Lugalo, Chifu Mkwawa hakutulia, bali aliendelea kuimarisha himaya yake pamoja na jeshi lake. Lakini pia kipindi hicho Wajerumani nao walikuwa wakipanga mikakati ya namna ya kuisambaratisha himaya hiyo.
Kitendo cha kupigwa kwa jeshi lao imara lenye silaha kali, tena na wapiganaji wenye mikuki na mishale tu, kiliichanganya Berlin kwa sababu hakikuwahi kutokea hapo kabla. Hivyo Gavana Julius Freiherr von Soden aliyekuwa anaongoza koloni hilo la Afrika Mashariki alikuwa katika presha kubwa kutoka kwa wakubwa wake kuhusiana na namna atakavyomshinda Mkwawa.
Gavana huyo alijitahidi kukabiliana na presha ya Wahehe waliokuwa wakivamia misafara yake hadi miaka miwili baadaye alipoondoka nchini. Wajerumani walikuwa na mbinu ya kuidhoofisha himaya ya Wahehe kwa mazungumzo, siyo kwa vita, kwa sababu walitambua kwamba hiyo ingeweza kuwagharimu tena.
Historia inaeleza kwamba, uamuzi wa Von Soden wa kutotumia jeshi kupambana na Mkwawa ulimfanya aonekane gavana bomu kati ya magavana wote walioongoza koloni hilo, lakini hiyo ilitokana na historia yake. Yeye ndiye alikuwa gavana pekee aliyetokea uraiani, kwani aliyemtangulia von Wissmann na wafuasi wake wa baadaye walikuwa makamanda wa jeshi.
Katika kipindi hicho cha Von Soden, Mkwawa naye alifanya majaribio kadhaa ya mazungumzo na Wajerumani akituma ujumbe wake Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalichukua muda wa miezi kadhaa kupitia kwa wawakilishi wake, lakini hayakuwa na mafanikio kwa sababu watawala wa Kijerumani walikuwa na mashaka na msimamo wa Mtawala huyo wa Wahehe kwamba angeweza kuwabadilikia. Kwa kifupi, hawakumwamini.
Pamoja na Von Soden kuwa na nia njema ya kufanya mapatano, maofisa wengine wa Kijerumani walikuwa na mawazo kwamba hakukuwa na haja yoyote ya kufanya mazungumzo na mtawala wa Kiafrika ambaye alikuwa ameidhalilisha Ujerumani kama alivyofanya Mkwawa.
Luteni Tom von Prince (baadaye Kapteni baada ya kuiangusha Kalenga) aliwahi kusema: “Tangu kuangushwa kwa kikosi cha Zelewski, hasa nikiwa askari wa jeshi lile la zamani, haja yangu kubwa ilikuwa kulipa kisasi kwa kudhalilishwa kwa jeshi letu, na tangu hapo nikaweka mkakati, sikuhitaji kuingia kwenye vita yoyote, sikufanya chochote ambacho kingeweza kuingilia kati mpango huu.”
Wajerumani wakati huo walikuwa na mashaka kwamba watawala wa Kiafrika, hususan Mkwawa walikuwa wameanza kuonyesha upinzani wa wazi, hasa Mtemi Isike wa Tabora na Mbunga wa Ungoni ambao himaya zao zilipakana na Uhehe. Chifu mmoja wa Usagara aliwahi kutamka wazi, “Watu hawa (Wahehe) ndio pekee walioweza kuoga mchanga wa damu ya Mzungu ambao ‘bomba zao za moto’ ziliwafanya wengi washindwe kujitetea. Na kweli, vijiji vingi vilivyokuwa jirani na boma la Wajerumani viliendelea kutoa msaada kwa Mkwawa na Himaya yote ya Uhehe mpaka pale Kalenga ilipoangushwa.
Sababu za Mkwawa kutochukua uamuzi wa kuwafukuzia wajerumani baada ya vita ya Lugalo zinatajwa kuwa nyingi. Itaendelea
No comments:
Post a Comment